Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga leo Jumatatu wanaongoza mkutano wa wabunge wa muungano tawala wa Kenya Kwanza na chama cha ODM.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki ni miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Uongozi cha KCB mtaani Karen.

Miongoni mwa yatakayozungumziwa wakati wa mkutano huo ni uendeshaji wa serikali jumuishi.
Chama ODM kiliridhia kuunda serikali jumuishi na utawala wa Kenya Kwanza baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z kuitikisa nchi kuanzia mwezi Juni mwaka jana.
Aidha, utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Maridhiano ya Kitaifa, NADCO utaangaziwa.
Ruto na Raila waliunda timu ya kusimamia utekelezaji wa ripoti hiyo siku chache zilizopita.
Wakati akizigumza huko Homa Bay wiki jana, Raila aliashiria kuwa yuko tayari kumuunga mkono Rais Ruto kuwania tena muhula wa pili kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Wawili hao walikuwa mahasimu kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, uchaguzi ambao Ruto alimbwaga Raila na kushinda urais.