Rais William Ruto amesema alichaguliwa kuiongoza nchi hii kutokana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Amesema kuna watu ambao hadi hii leo hawaamini kwamba alichaguliwa kuwa Rais wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 licha ya yeye kuwa mtu wa kawaida.
“Hata mimi ni mtu tu wa kawaida. Nimefika hapa kwa mapenzi ya Mungu. Kuna watu walikuwa na matatizo sana, hata saa hizi bado hawajaamini mimi ni Rais, bado wanahangaika. Lakini Mungu ni nani Bwana?” Alisema Rais Ruto wakati akihutubia Klabu ya Soka ya Nairobi United, ambayo ni mshindi wa Kombe la Mozzart Bet katika Ikulu ya Nairobi leo Alhamisi.

“Mimi ndio niko hapa kwa sasa. Wajipange. Mimi ndio niko hapa kwa sasa kwa mapenzi ya Mungu, I am here,” aliongeza Rais Ruto wakati wa hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja.

Kauli za Ruto zikija siku moja baada ya yeye kutoa onyo kali kwa viongozi wa upinzani dhidi ya kile alichokitaja kuwa njama ya kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wake.
“Kama wako na mpango, tukutane 2027. Lakini njia ya mkato hapa katikati, hakuna. Nchi hii haitaharibiwa na watu wachache ambao hawana subira na wanataka kubadili serikali kutumia njia zisizokuwa za kikatiba,” alionya Rais Ruto Julai 9 wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba 542 katika kituo cha polisi cha Kilimani katika eneo bunge la Dagoretti Kaskazini, jijini Nairobi.
Kwa upande wake, upinzani ukiongozwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua umekanusha madai ya kutaka kuupindua utawala wa Kenya Kwanza ukisema lengo lao ni kumbandua Ruto madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Ilivyo kwa sasa, pande zote za kisiasa zimeanza kunoa makali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wakati mashaka yakiongezeka kuwa kukawia kuwaapisha makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC huenda kukawa na athari kubwa kwa maandalizi ya uchaguzi huo.
Mahakama ilitarajiwa kutoa uamuzi juu ya kesi iliyowasilishwa kupinga kuapishwa kwa makamishna hao leo Alhamisi.