Ruto kwa Maraga: Utakuwaje Rais wa nchi iliyofeli?

Jaji Mkuu mstaafu David Maraga yuko mbioni kukusanya fedha kutoka kwa Wakenya zitakazomwezesha kufanya kampeni kali kwa lengo la kumbandua Rais Ruto madarakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto ametilia shaka azima ya Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Ruto ameshangaa namna Maraga atakavyoongoza nchi anayodai imefeli.

“Nilimsikia muungwana fulani aliyestaafu siku chache tu zilizopita akisema Kenya ni nchi iliyofeli na nikashangaa jinsi anavyotaka kuwa Rais wa nchi iliyofeli,” alisema Rais Ruto aliyezungumzia kwa mara ya kwanza juhudi za Maraga kutaka kumbandua madarakani kwenye uchaguzi ujao.

“Unataka tukuamini kwa kukupa uongozi wa nchi ambayo hata hauna imani nayo?”

Si hayo tu, kiongozi wa nchi pia amewakosoa wapinzani wake anaosema hawana ajenda yoyote ya kuifaidi nchi kando na kutumia maneno ya  kuvutia kama vile Wantam.

“Kwa wale wanaoeneza maneno ya kuvutia yanayosema “Ruto must go,” “Kasongo,” “Wantam,” au maneno yoyote yale wanaotumia hii leo, Rais hakosi lepe la usingizi na kama tu watangulizi wake, muda wake wa kuondoka utawadia. Hiyo ni dhahiri. Kwa hivyo, hebu tuzungumze mambo ya msingi na hii ndio changamoto ya kweli: Kando na maneno hayo, mpango wenu ni upi?

Awali, Ruto aliwapuuzilia mbali wapinzani wake kwa kucheza siasa za uchochezi na ukabila bila ya kuwa na mpango madhubuti wenye manufaa kwa nchi.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Maraga yuko mbioni kukusanya fedha kutoka kwa Wakenya zitakazomwezesha kufanya kampeni kali kwa lengo la kumandua Rais Ruto madarakani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article