Utawala wa Kenya Kwanza umekusudia kusuluhisha changamoto mbalimbali zinazowakumba Wakenya kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo umekuwa madarakani.
Rais William Ruto amesema azma ya Wakenya ni kuona ufumbuzi wa kivitendo kwa changamoto zinazowakumba wakati wakiishi viwango bora vya maisha.
Azma ambayo kiongozi wa nchi anasema serikali yake imelivalia njuga hadi kufikia sasa.
“Tumeufanya uchumi kuwa thabiti, tumeufanyia mtungo wa thamani ya kilimo mabadiliko, tumehakikisha upatikanaji wa afya kwa wote kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii na kutekeleza sera za kimakusudi ili kubuni nafasi za ajira kwa vijana,” aliongeza Rais Ruto.
“Ili kuongezea kwa mafanikio haya, tunafanya kazi na viongozi wanaopenda maendeleo kutoka mirengo yote ya kisiasa kuimarisha umoja wa taifa.”
Ruto aliyasema hayo leo Alhamisi alipokutana na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Migoro katika Uwanja wa Sony Sugar mjini Awendo.

Gavana wa Migori Ochillo Ayacko, wabunge na wawakilishi wadi ni miongoni mwa waliokuwapo.
