Rais William Ruto amesema kuna haja ya kukomesha mara moja zimwi la ufisadi lililokithiri bungeni la sivyo litatishia mustakabali wa taifa.
Ametoa mfano wa mjumbe ambaye hakumtaja kwa jina na anayesema alipokea rushwa ya kitita cha shilingi milioni 150.
“Mtu anatoa wapi shilingi milioni 150? Hizo ni pesa za nchi,” alisema Ruto wakati wa mkutano wa wabunge wa ODM na Kenya Kwanza mtaani Karen.
“Wanachama wachache wa kamati yenu walipokea shilingi milioni 10 ili kuipinga sheria ya kupambana na utakatishaji fedha,” alisema Rais Ruto akipuuzilia mbali madai ya baadhi ya wabunge kwamba ufisadi haujakithiri kwenye taasisi hiyo.
Kongozi wa nchi amelalama kuwa kuna baadhi ya wabunge wanaoliharibia bunge sifa kwa kusingizia kukusanya fedha kwa niaba ya bunge, fedha ambazo huishia kuwanufaisha wao wenyewe.
Ameapa kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kushtakiwa kutokana na mienendo yao.
“Kuna tatizo. Ikiwa hatutalikomesha tatizo hili, tunaenda kuiharibu nchi yetu,” alionya Ruto.
Ni kauli ambazo zimeungwa mkono na kinara wa ODM Raila Odinga.
Raila akisema kuwa kamati za bunge hutumiwa kuitisha hongo kutoka kwa watu na mashirika yanayofika mbele yake.
Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, kiongozi wa walio wachache katika Bunge la Taifa Junet Mohamed alikanusha kuwa ufisadi umetalaki katika kamati za bunge.
Hali iliyomfanya Rais Ruto kumjibu akisema kama kiongozi wa nchi, yeye hupata taarifa ghafi za kijasusi, na kwa misingi hiyo, anafahamu anachokisema.
Mara ya kwanza kwa Ruto kusema ufisadi umekitihiri bunge ilikuwa wakati wa Kongamano la Ugatuzi lililofanyika katika kaunti ya Homa Bay wiki jana.
Ni hali iliyowachochea baadhi ya viongozi wa kamati hizo kumtaka kiongozi wa nchi kuthibitisha madai yake.
Changamoto ambayo ameonekana kuichangamkia kwa kutaja kiasi cha fedha zilizohusika hata ingawa hakuwataja wahusika.
Wakati wa mkutano huo, wote hao walizungumzia azimio la ushirikiano wao wakielezea jinsi walivyoamua kuzika tofauti zao kwa manufaa ya taifa.
“Ruto na mimi tuliamua kwamba ni bora kuwa na nchi yenye dosari ambayo inahangaika kurekebisha mienendo yake kuliko ile iliyosambaratika,” alisema Raila wakati akihutubia mkutano huo.
Viongozi hao wawili wameahidi kuhakikisha ripoti ya Kamati ya Maridhiano ya Kitaifa, NADCO inatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya nchi.