Ruto kuizawadi Harambee Stars shilingi milioni 600 iwapo itashinda CHAN

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto aiandalia timu ya Harambee Stars dhifa ya asubuhi katika Ikulu ya Nairobi.

Rais William Ruto ameahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni 600 kwa timu ya taifa ya soka Harambee Stars iwapo itashinda kombe la CHAN 2024.

Wakati huo huo, kiongozi wa taifa aliahidi timu hiyo kitita cha shilingi milioni 60 iwapo itatinga robo fainali, shilingi milioni 70 iwapo itafika nusu fainali na shilingi milioni 90 iwapo itafuzu kwa fainali.

Rais alisema kila mchezaji atapokea shilingi milioni moja kwa kila mchuano watakaoshinda na shilingi nusu milioni kwa kila mchuano watakalotoka sare.

“Tumeongeza zawadi mara tatu ili kila mchezaji atie bidii zaidi,” alisema Rais Ruto.

Aliyasema hayo leo Jumamosi alipoiandalia timu hiyo dhifa ya kiamshakinywa katika hoteli ya Pullman jijini Nairobi, kabla ya mechi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC siku ya Jumapili.

Michuano ya kuwania ubingwa wa CHAN itakayodumu mwezi mmoja na kuandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania, itaanza leo Jumamosi jijini  Dar es Salaam, Tanzania.

Rais Ruto amewahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi na kuishabikia Harambee Stars.

Alimtaka kila Mkenya kuifanya Harambee Stars kuwa chama chake cha kisiasa.

“Tuweke kando vyama vyote vya kisiasa, chama chetu cha kisiasa mwezi huu ni Harambee Stars,” alidokeza Rais Ruto.

Share This Article