Mtu yeyote atakayejihusisha katika visa vya ufisadi atakabiliwa vikali kisheria bila kujali hadhi yake katika jamii.
Rais William Ruto amelalamika kuwa jinamizi la ufisadi limekuwa mwiba kwa juhudi za serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Amesema vita dhidi ya ufisadi vitafanikiwa tu ikiwa kila mtu katika jamii atahusika katika kuvikabili.
Kulingana naye, mapambano dhidi ya uovu huo yanapaswa kuimarishwa zaidi bila kujali hadhi ya wahusika ikiwa ni pamoja na bunge na magavana.
Ruto amezinyoshea mkono wa lawama kamati za bunge anazosema huwa na mazoea ya kuitisha rushwa ili kuandaa ripoti zinazowapendelea wanazozitoa rushwa hizo.
Wakati huohuo, ameikosoa Idara ya Mahakama kwa kuwa mstari wa mbele kutoa dhamana za kuzuia kukamatwa kwa wanaohusika katika visa vya ufisadi.
“Kuna kitu kinaitwa dhamana ya kuzuia kukamatwa kwa wanaohusika katika ufisadi. Hicho ni kitu kilichobuniwa nchini Kenya kuwalinda wafisadi,” alilalama kiongozi wa nchi aliyeapa kukabiliana vikali na zimwi hilo.
Sasa anatoa wito kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC kujibidiisha katika kuhakikishia wafisadi wote wanawajibishwa.