Ruto asisitiza umuhimu wa elimu inayokidhi mahitaji ya soko la ajira duniani

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wakati akiwahutubia Wakenya wanaoishi nchini Misri
Rais William Ruto amesema Kenya imedhamiria kuhakikisha kiwango cha masomo yanayotolewa nchini kinakidhi mahitaji ya soko la ajira duniani. 
Ruto amesema soko la sasa linahitaji maarifa madhubuti, ujuzi na umilisi unaokidhi mahitaji na viwango vya waajiri na sekta mbalimbali.
Akiwahutubia Wakenya katika hoteli moja jijini Cairo nchini Misri jana Jumatano jioni, Ruto alisema Kenya ina rasilimali watu bora kote duniani.
“Kila mahali ninakoenda, naambiwa Wakenya wananawiri na wanahitaji usimamizi mdogo katika kile wanachokifanya,” alisema.
Rais aliongeza kuwa serikali inatilia mkazo uboreshaji wa matokeo ya rasilimali watu akidokeza kuwa shilingi bilioni 650 ambazo ni sawa na dola bilioni 5 zinatumiwa katika kuwaelimisha na kutoa mafunzo kwa Wakenya kutoka kiwango cha chini hadi chuo kikuu.
Ruto alisema aliteua Jopokazi la Rais Juu ya Mageuzi ya Elimu alipoingia madarakani ili kupitia upya mfumo wa elimu nchini na kutoa mapendekezo ya namna ya kuiboresha sekta hiyo.
“Tunatekeleza mapendekezo na tumeona mabadiliko makubwa katika vyuo vikuu vyetu na utoaji mafunzo ulioboreka,” alisema Rais.
Aliongeza kuwa serikali imeajiri walimu 76,000 katika kipindi cha miaka miwili, ishara tosha kuwa mageuzi katika sekta ya elimu yanazaa matunda licha ya kukabiliwa na changamoto.
Wakati huohuo, Ruto alipongeza wajibu muhimu unaotekelezwa na Wakenya wanaoishi ughaibuni katika maendeleo ya taifa na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa Kenya.
Amesema serikali inaweka umuhimu mkubwa kwa raia wake wanaoishi ughaibuni na inatambua uhusiano wa karibu walio nao na nchi yao ya nyumbani.
Kuhusiana na uhusiano mzuri kati ya Kenya na Misri, Rais Ruto alisema nchi hizo mbili zinajivunia uhusiano mzuri katika nyanja mbalimbali akiongeza kuwa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika ni mwagizaji mkubwa wa majani chai kutoka Kenya.
Share This Article