Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, UN Ban Ki-mmon ametunukiwa tuzo kuu zaidi humu nchini katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.
Rais William Ruto alimtunuku Ban tuzo ya Chief of the Order of the Golden Heart (C.G.H.) kutokana na mchango wake mkubwa katika kuleta mabadiliko katika masuala ya kimataifa na binadamu kwa kipindi chake cha zaidi ya miaka 50 ya utumishi wa umma.
Akimtunuku tuzo hiyo, Rais Ruto alisema wakati wa uongozi wake kama Katibu Mkuu wa UN, Ban aliuhamasisha ulimwengu kukabiliana na changamoto za kimataifa kuanzia kwa mabadiliko ya tabia nchi, afya ya dunia na ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake, Ban alimshukuru Rais Ruto na kupongeza jitihada zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Makao makuu mapya ya Kituo cha Kimataifa cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi yamepangiwa kuanzishwa jijini Nairobi.