Rais William Ruto leo Jumatatu amekabidhi rasmi Hati kamili ya utambuzi wa chuo kikuu kwa chuo cha Gretsa.
Alitaja tukio hilo kuwa hatua ya kihistoria kwa taasisi hiyo na kwa sekta ya elimu ya juu nchini kwa jumla.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi, Rais alisema mafanikio hayo yanaonyesha jukumu muhimu la vyuo vikuu vya kibinafsi la kupanua upatikanaji wa elimu bora na kuzalisha wahitimu faafu kwa mahitaji ya soko la ajira.
Chuo kikuu cha Gretsa kilichoanza kupokea wanafunzi wa kwanza wa shahada mwaka 2006, sasa ni chuo kikuu cha kibinafsi cha 31 nchini, kupokea hati kamili ya utambuzi.
Taasisi hiyo imeeandaa mahafali 13 na kuzalisha zaidi ya wahitimu 8,500 katika viwango vya cheti, diploma na shahada, idadi ambazo Rais Ruto alisema zinaonyesha ukuaji wake thabiti na mchango wake kwa taifa.
Ruto alibainisha kuwa Kenya sasa ina vyuo vikuu 82 vilivyoidhinishwa, 45 vya umma na 37 vya kibinafsi ishara kwamba mazingira ya elimu ya juu yanayobadilika kwa kasi.
Alisema hati hiyo inaashiria ushirikiano wenye mafanikio kati ya serikali na sekta binafsi katika kuhakikisha viwango vya juu vya kielimu na kupanua fursa za masomo.
Rais alivitaka vyuo vikuu kujiandaa kwa kundi la kwanza la wanafunzi wa mfumo wa umilisi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu mwaka 2029.
Alivihimiza kufanya hivyo kwa kukumbatia mbinu mpya za kufundisha, kuimarisha mafunzo ya vitendo na kuwajengea uwezo wahadhiri.
Pia alizitaka taasisi kujumuisha akili bandia katika kufundisha, utafiti na uendeshaji, akisisitiza Mkakati wa Kitaifa wa AI wa 2025–2030.