Mwanamuziki wa Nigeria Paul Okoye maarufu kama Rudeboy ametangaza masharti makali kwa wanamuziki wanaotaka kusajiliwa kwenye kampuni yake iitwayo Fire Department Inc.
Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alisema kila msanii anayetaka kujiunga na kampuni hiyo ni lazima atoe dhamana ya mali isiyoweza kuhamishika.
Masharti mengine aliyotaja msanii huyo ni pamoja na mkataba wa msanii kuhusisha sahihi ya mzazi au mlezi wake na msanii kulipa faini ya Naira milioni 10 endapo atakamatwa akivuta bangi au kutumia dawa nyingine za kulevya.
Rudeboy ambaye awali alikuwa mmoja wa wasanii wawili wa kundi la muziki la P Square alisema wasanii wakipata umaarufu huwa wanajisahau wanasharau kampuni zilizowasajili.
Kulingana naye, masharti haya yatahakikisha wasanii wanadumisha nidhamu na uwajibikaji.
“Watu wanaamini wamekua wakubwa kuliko lebo ya muziki. Kwa hiyo nitakuambia mahitaji yangu sasa. Utahitajika kuleta mali isiyohamishika, wazazi wako watasaini. Siku nitakapokukamata ukivuta kitu, utalipa Naira milioni 10” alisema Rudeboy.
Fire Department Inc. ilianzishwa mwaka 2019, miaka miwili baada ya kuvunjika kwa kundi la P-Square. Ingawa Rudeboy na ndugu yake Peter Okoye walijaribu kurudisha ushirikiano wao mwaka 2021, walitengana tena.
Wanamitandao wana maoni tofauti kuhusu masharti hayo ambapo wengine wanayaunga mkono kwani yatahakikisha nidhamu huku wengine wakionelea kwamba ni magumu na huenda yakawa kikwazo kwa baadhi ya wasanii chipukizi.