Kundi la waasi la RSF nchini Sudan limevamia shule ya chekechea na maeneo mengine katika eneo la Kalogi, jimbo la Kordofan Kusini na kuua angalau watu 116, kulingana na afisa wa eneo hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa eneo la Kalogi alielezea wanahabari Jumamosi kwamba waathiriwa wa shambulio hilo walijumuisha watoto 46 waliokuwa wakihudhuria shule hiyo ya chekechea.
Vyanzo viwili vya kijeshi katika Jeshi la serikali ya Sudan pia viliiambia wanahabari kwamba RSF ilishambulia shule ya chekechea Alhamisi na baadaye kulenga raia waliokusanyika kutoa msaada baada ya mauaji hayo.
Hospitali ya jiji hilo na jengo la serikali pia zililipuliwa, kulingana na vyanzo hivyo.
Ukosefu wa mawasiliano katika eneo hilo umefanya iwe vigumu kuripoti idadi kamili ya vifo, lakini kulikuwa na hofu kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi, vyanzo hivyo viliongeza.
“Mauaji ya watoto katika shule yao ni ukiukaji wa kutisha wa haki za watoto” alilalama Sheldon Yett, mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu watoto, UNICEF, nchini Sudan, katika taarifa iliyotolewa Ijumaa.
Yett aliongeza kwamba watoto hawapaswi kulipa gharama ya mgogoro, akizitaka pande zote kusitisha mashambulio haya mara moja na kuruhusu upatikanaji salama na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa walio na mahitaji makubwa.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulikuwa umeripoti awali Alhamisi kwamba angalau watu tisa waliuawa, wakiwemo watoto wanne na wanawake wawili, katika mashambulio ya makusudi ya droni yaliyofanywa katika mji wa Kalogi na RSFna mshirika wake, Sudan People’s Liberation Movement–North (al-Hilou), dhidi ya shule ya chekechea na taasisi kadhaa za kiraia.