Rosemary Odinga, binti mkubwa wa Raila Amolo Odinga amesimulia kuhusu jinsi alifahamu kuhu kifo cha babake mzazi Raila Amolo Odinga.
Akizungumza uwanjani Nyayo wakati wa ibada ya wafu kwa ajili ya marehemu babake, Rosemary alisema siku hiyo ambayo ni Oktoba 15, 2025, alikuwa nyumbani kwake punde baada ya kupata kiamsha kinywa.
“Nilikuwa nyumbani nimekaa kwa meza, muda mfupi baada ya ula kiamsha kinywa, nikapigiwa simu na ndugu yangu Raila Junior,” alielezea Rose akiwa ameandamana na binti zake.
Rosemary anasema kwanza Junior alitaka kufahamu alipokuwa kisha akamtaka aketi chini labda kwa sababu ya uzito wa ujumbe ambao alikuwa anakaribia kumpa.
Alishangaa iwapo alitakiwa aketi chini sakafuni au vipi kwani tayari alikuwa amemwambia Junior kwamba ameketi, akisema kwa muda huo mfupi alichanganyikiwa sana lakini hapo hapo akampa ujumbe kwamba baba yao amefariki.
Tofauti na wenzake, Rosemary hakuwa ameandika hotuba ya kusoma leo kwenye ibada ya wafu ya babake akisema kwamba hakutarajia kwamba angezungumza leo.
Aliombea wakenya nguvu kutoka kwa Mungu pamoja na familia yake wakati huu mgumu.
Zaidi ya kuwa babake mzazi, Rosemary alisema mwendazake Raila Amolo Odinga alikuwa mshauri wake na mtu ambaye alimwelewa sana yeye na ndugu zake.