Ronaldo anyakua Kombe la tatu la Ulaya na Ureno

Timu hizo zilitoka sare ya 2-2 katika dakika 120 na kubidi mshindi atafutwe kupitia changamoto ya matuta.

Dismas Otuke
1 Min Read

Ureno iliwashinda  Uhispania mabao 5-3, kupitia mikiki ya penati katika fainali ya kombe la UEFA Nations League, Jumapili usiku ugani Allianz Arena nchini Ujerumani.

Timu hizo zilitoka sare ya 2-2 katika dakika 120 na kubidi mshindi atafutwe kupitia changamoto ya matuta.

Martin Zubimendi alifungua ukurasa kwa Uhispania kwa bao la dakika ya 21, kabla ya Nuno Mendes kusawazisha kwa Ureno dakika 5 baadaye.

Mikel Oyarzabal aliwaweka Uhispania uongozini kunako dakika ya 45, kipindi cha kwanza kikiishia kwa uongozi wa Uhispania wa 2-1.

Ureno ilirejea mchezoni dakika ya 61 kupitia kwa nahodha Cristiano Ronaldo, na mechi ikamalizikia kwa sare ya 2-2 baada ya dakika 120.

Goncalo Ramos, Vitinha, Bruno Fernandes, Nuno Mendes, and Reuben Neves walipachika penati zote tano, huku Mikel Merino, Alex Baena, na Isco wakiifungia Uhispania, wakati mkwaju wa Alvaro Morata, ukipanguliwa na kipa Diogo Costa wa Ureno.

Ronaldo anajivunia kunyakua kombe la Euro na Ureno mwaka 2016 kabla ya kushinda Kombe la UEFA Nations League mwaka 2019 na la pili jana usiku.

Ufaransa iliwapiku wenyeji Ujerumani mabao 2-0 na kunyakua nishani ya shaba.

Share This Article