Romy Jons kuwania ubunge Mbagala

Haya yalibainika baada ya Romy kuchukua fomu za uwaniaji kutoka kwa afisi za CCM.

Marion Bosire
1 Min Read

Mpiga muziki wa Tanzania yaani Dj Romy Jons atawania ubunge wa eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, kupitia chama tawala cha CCM.

Hii ni baada ya kaka huyo wa mwanamuziki tajika Diamond Platnumz kuchukua fomu za uwaniaji huo kutoka kwa afisi za chama cha CCM za Wilaya ya Temeke mtaani Taifa Pub, jijini Dar es Salaam.

Jons hajatoa tamko lolote kuhusu hatua aliyochukua lakini ikumbukwe kwamba amekuwa katika mstari wa mbele katika kumpigia debe Rais Samia Suluhu Hassan kwa uchaguzi huo unaokuja.

Diamond Platnumz anaonekana kuridhishwa na hatua aliyochukua kakake huku akisema kwamba ana imani naye kabisa.

Msanii huyo ameahidi pia kumuunga mkono Romy Jons kwa hali na mali ili kuhakikisha kwamba anahudumia watu wa Mbagala ipasavyo na kuwaletea maendeleo.

“Labda tu chama kisikupe nafasi” alimalizia Diamond ujumbe wake kwenye Insta Stories ambao unaonyesha imani kubwa aliyo nayo ya kakake kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Tanzania itaandaa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025 na wasanii kadhaa wamejitokeza kuwania nyadhifa za kuchaguliwa akiwemo Harmonize.

Harmonize naye alitangaza kuwania ubunge wa eneo la alikozaliwa la Tandahimba katika mkoa wa Mtwara, nchini Tanzania, lakini hajatangaza iwapo amechukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Share This Article