Mwanamuziki Alex Nyachonga Apoko, almaarufu Ringtone, alifikishwa katika mahakama ya Milimani baada ya kuhusishwa na sakata ya ardhi ya kitita cha shilingi Milioni 50 mtaani Runda.
Rington anadaiwa kutoa habari za uwongo na kujaribu kumiliki hekari 0.1908 ya ardhi katika mtaa wa Runda Jijini Nairobi.
Mlalamishi katika kesi hiyo, alidai kuwa Ringtona akiwa ameandamana na kundi la wahuni, alivamia ardhi hiyo na kumfurusha mfanyakazi aliyekuwa akiilinda na kisha kumili ardhi hiyo, hatua iliyomsababisha kuripoti kisa hicho kwa maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema mlalamishi huyo ambaye ni mwanamke kisha alifika mahakamani katika juhudi za kutaka arejeshewe ardhi yake.
Kitengo cha DCI cha kushughulikia kesi za ardhi kilianzisha uchunguzi na kubainisha kuwa Rington na washirika wake walimhadaa mwathiriwa kwa kujaza hatia bandia ya kiapo Februari 28, 2023. Katika hati hiyo ya kiapo mwanamuziki huyo alidai kuwa yeye ndiye mmiliki halisi wa ardhi hiyo, akidai amekuwa akiishi katika ardhi hiyo kwa muda wa miongo miwili.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kina, maafisa hao walibainisha kuwa mlalamishi ndiye mmiliki halisi wa ardhi hiyo tangu Machi 14,2000.
Mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rington na baada ya kuwahepa maafisa wa usalama kwa muda wa wiki kadhaa, hatimaye alikamatwa kutoka kwa maficho yake mtaa wa Kasarani, na kufikishwa mahakani akishtakiwa kwa kutoa habari za uwongo.
Alikanusha mashtaka dhidi yake lakini akanyimwa dhamana na anazuiliwa katika gereza la viwandani akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu ambapo kesi ya kutaka kuachiliwa kwa dhamana itasikizwa.