Mwanamuziki nyota wa Marekani na mfanyabiashara Rihanna ametangaza kuzaliwa kwa mwanao wa tatu wa kike na mpenzi wake A$AP Rocky.
Mmiliki huyo wa Fenty Beauty alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ambapo alichapisha picha inayomwonyesha akiwa amempakata mtoto huyo.
Hakuweka maneno mengi chini ya picha hiyo ila ni jina ambalo ni Rocki Irish Mayers na tarehe inayoaminika kuwa ya kuzaliwa kwake ambato ni Septemba 13, 2025.
Chapisho hili limezima uvumi ambao umekuwa ukienea mitandaoni ambapo kwa siku kadhaa zilizopita, watu walikuwa wakikisia kwamba tayari amejifungua.
Rihanna na A$AP Rocky walijaliwa mwanao wa kwanza wa kiume kwa jina RZA Athelston Mayers Mei ya 2022. Mwanao wa pili ambaye pia ni mvulana kwa jina Riot Rose Mayers,alizaliwa Agosti 2023.
Mwanamuziki huyo wa asili ya Barbados wa umri wa miaka 37, amewahi kuzungumza awali kuhusu uzazi akielezea jinsi umebadili maisha yake huku akiurejelea kuwa kitu bora zaidi kuwahi kutokea kwa maisha yake.
Hata ingawa Rihanna amechukua mapumziko marefu katika muziki tangu mwaka 2016 alipotoa albamu iitwayi Anti, amesalia kuwa nguvu muhimu katika tasnia ya mitindo ya mavazi na bidhaa za urembo kupitia kwa kampuni yake ya Fenty.