Msanii wa muziki na mfanyabiashara Rihanna ametangaza kwamba yeye ndiye ameangaziwa kwenye toleo la 14 la jarida maarufu la Hommegirls.
Rihanna au ukipenda Riri alichapisha picha alizopigwa kwa ajili ya jarida hilo kwenye akaunti yake ya Instagram huku akitangaza tarehe ya kuzinduliwa kwa mavazi aliyotumia kwenye toleo hilo.
Tangazo lake linamtaja Gabriel Moses kama mpiga picha huku Stella Greenspan akitajwa kuwa msanifu mavazi aliyehusika akitumia mavazi ya kampuni ya Rihanna iitwayo FENTY na yale ya kampuni ya PUMA.
Mavazi hayo yatazinduliwa rasmi tarehe 23 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025.
Hommegirls ni jarida la mitindo ya mavazi linalochapishwa mara mbili kwa mwaka na ni falsafa ya mitindo inayosherehekea mtindo wa androjeni na kuchunguza dhana ya “uume ndani ya uanamke” kupitia mitindo ya wanawake iliyochochewa na mitindo ya wanaume.
Jarida hili na falsafa yake vimejengwa juu ya wazo kwamba wanawake wanaweza kuamsha uanamke wao kwa kuvaa mavazi yanayochukuliwa kuwa ya kiume.
Linasisitiza ushonaji wa hali ya juu, mitindo ya mtaani, sare na mavazi ya lazima kutoka kwa chapa za urithi na mitindo ya mitaani, pamoja na makala yanayochochea fikra, mahojiano na picha za mitindo zinazohusu utamaduni na jinsia.