Regina Daniels asifia muungano wa wazazi wake kwa ajili yake

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa filamu nchini Nigeria Regina Daniels amesifia muungano wa wazazi wake ambao walishatengana kwa ajili ya furaha yake.

Regina alichapisha picha na video za wazazi wake wakiwa pamoja na kuandika, “Maadui wawili waliokwisha kumalizana wanaungana tena bila malengo mabaya ila kwa ajili ya furaha ya binti yao.”

Binti huyo aliendelea kushangaa iwapo anafaa kulalamikia hali aliyojipata kwa sasa.

Wazazi hao walisafiri hadi jijini Abuja kutafuta kuachiliwa huru kwa mwanao wa kiume aitwaye Sammy ambaye anadaiwa kukamatwa kwa amri ya mume wa Regina, Seneta Ned Nwoko.

Regina alikorofishana na Ned akaondoka kwake akakomboa nyumba ambayo anaishi na watu wa familia yake na ainaripotiwa kwamba Ned aliamua kukamata watu wa karibu na Regina kama njia ya kumshurutisha arejee kwake.

Mwigizaji huyo aliyeanza kuigiza akiwa mtoto mdogo anasema inachukua muda kupata uhuru wa Sammy lakini ana imani kwamba mwishowe atakuwa huru.

Ametishia kwenda mwenyewe alikozuiliwa kakake akisema, “Nitaenda huko mwenyewe na nisababishe dhoruba! Si wananitaka mimi! Babangu ni wakili. Mmoja wa mawakili wakubwa enzi hizo lakini yakatokea.”

Alimsifia pia mamake mzazi akisema pamoja na babake wamejitolea kikamilifu kwa furaha ya watoto wao.

Sakata ya Regina na Ned Nwoko ilianza baada ya video kusambaa mitandaoni ikimwonyesha Regina aliyejawa ghadhabu akidhibitiwa na watu wanaoaminika kuwa wafanyakazi.

Alisikika akisema, “Kwetu mimi nachukuliwa kuwa malkia lakini kwa nyumba ya Ned Nwoko mimi si kitu”. Baadaye picha zilisambaa mitandaoni zinazoonyesha jinsi Regina aliharibu vitu nyumbani kwa Ned kabla ya kuondoka.

Ned alitoa taarifa akisema kwamba Regina alikuwa ameingilia matumizi ya mihadarati na anataka kumpeleka katika kituo cha kurekebisha tabia.

Regina amekanusha kabisa madai ya kuwa mraibu wa mihadarati.

Share This Article