Raven Symone aliyeanza kuigiza akiwa mtoto mdogo nchini Marekani amezungumzia urithi wenye utata wa Bill Cosby, mchekeshaji na mtayarishaji aliyempa jukwaa la kuendeleza kipaji chake kwenye kipindi cha “The Cosby Show”.
Symone ambaye mara nyingi hapendi kuzungumza hadharani aligusia athari za kitamaduni na makosa ya kingono aliyohusishwa nayo Bill Cosby akisema yeye huchagua makusudi kuweka mpaka kati ya mazuri ya mtu na mtu mwenyewe.
Alikuwa akihojiwa kwenye kipindi cha mitandaoni cha “Hate to Break It to Ya” naye Jamie Kennedy, ambapo aliulizwa jinsi yeye humchukulia msimamizi wake wa awali wakati huu anakumbwa na matatizo ya kisheria.
Raven Symone aliigiza kama Olivia Kendall kwenye kipindi hicho cha vichekesho cha Cosby kutoka mwaka 1989 hadi 1992.
Alisifia mchango wa kitaaluma wa Cosby katika tasnia ya burudani bila kujali matatizo yake akisema alibadili Marekani na vipindi vya runinga nchini humo.
Mawazo ya Symone ni dhihirisho la ugumu ambao wahusika wa tasnia ya burudani na umma kwa jumla hupitia katika kutambua kazi za mtu huku mtu huyo binafsi akikumbwa na matatizo ya kisheria.
Symone ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 39 hata hivyo alitambua kiwango cha madai ya makosa anayokumbwa nayo Cosby ambaye analaumiwa kwa kudhulumu kingono wanawake wapatao 60.
Cosby alihukumiwa mwaka 2018 kwa dhuluma mbaya za kingono kutokana na kesi ya mwaka 2004 inayomhusisha Andrea Constand ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani.
Mahakama ya upeo ya Pennsylvania hata hivyo, ilibatili uamuzi huo wa mahakama mwaka 2021 kwa misingi ya kimchakato na kusababisha kuachiliwa kwake baada ya miaka mitatu gerezani.