Msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Rapcha alijibu wito wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kufika katika afisi za Baraza hilo kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji, Dkt. Kedmon Mapana.
Wito wa msanii huyo kwa BASATA ulikuwa umechapishwa kwenye akaunti rasmi ya baraza hilo ukimwelekeza afike saa nne asubuhi leo.
Mara nyingi wasanii wakiitwa na baraza hilo huwa wamekiuka maadili na haikuwa tofauti kwa Rapcha.
Mazungumzo kati ya wawili hao yaliangazia maudhui ya video ya wimbo wake iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii wiki kadhaa zilizopita.
Katika kikao hicho, Rapcha aliomba radhi kwa BASATA na kwa Watanzania kwa maudhui ya wimbo huo huku akichukua hatua ya kuufuta katika account zake za mitandao ya kijamii.
Aidha, Msanii huyo alipokea Kitabu cha Maadili katika Kazi za Sanaa kilichotolewa na BASATA kama mwongozo wa kufuata katika kazi zake zijazo ambapo ameahidi kushirikiana kwa karibu na BASATA na kuwa Balozi mzuri wa kuhamasisha maadili bora katika tasnia ya sanaa Nchini.
Makosa yalitokea pale ambapo Rapcha alianza kutangaza wimbo wake mpya mitandaoni kwa kuchapisha picha zilizomwonyesha akiwa na mwanamke katika hali inayokiuka maadili kwani walikuwa kitandani.