Rais wa Marekani Donald Trump amepatiwa mapokezi ya kifalme baada ya kuwasili Saudi Arabia, kituo chake cha kwanza katika ziara ya siku tatu ambapo pia atazuru Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu – UAE.
Trump alisikika akisema “Tunapendana sana” wakati wa mazungumzo na Mwana wa mfalme Mohammed bin Salman huku akitarajia kupata uwekezaji wa dola trilioni moja katika viwanda vya Marekani.
Viongozi hao wawili pia wamekutana na wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa za Marekani ambao wako Riyadh kwa ajili ya kikao cha uwekezaji kati ya Saudi Arabia na Marekani.
Trump anatarajiwa kuzingatia zaidi kupata uwekezaji mkubwa wa kifedha kwa Marekani na kuimarisha diplomasia katika masuala ya kikanda.
Ikulu ya White House imesema kuwa Trump anafanya marejeo ya kihistoria katika eneo la mashariki ya kati, hii ikiwa ziara yake rasmi ya kwanza ya kitaifa katika muhula wake wa pili wa urais, ambapo atazingatia sana kuimarisha uhusian.
Rais huyo wa Marekani Trump na mwana wa kifalme Mohammed wanaripotiwa kutia saini mkataba wa maelewano, kulingana na video iliyoonyesha viongozi hao wawili wakisalimiana baada ya kusaini, huku wakipigiwa makofi na wajumbe wao.
Mazungumzo bado yanaendelea kati ya mwana wa kifalme Mohammed na Trump na yanazingatia zaidi kukamilisha mikataba mikubwa ya biashara na silaha ambayo itatangazwa baadaye leo.
Wana matumaini ya kufikia makubaliano ya pamoja ya usalama jambo ambalo Saudi Arabia ilijaribu kuafikia na utawala wa Biden.