Rais wa Marekani Donald Trump amekubali kuongeza muda wa kufanya mazungumzo kuhusu ushuru na Umoja wa Ulaya – EU hadi tarehe 9 mwezi Julai.
Hatua hii inajiri baada ya Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen kusema kwamba alikuwa na mazungumzo mazuri na Trump siku ya Jumapili kwa njia ya simu.
Mwezi uliopita, Trump alitangaza ushuru wa asilimia 20 kwa bidhaa nyingi kutoka EU, lakini baadaye akaupunguza kwa nusu hadi asilimia 10 hadi tarehe 8 mwezi Julai ili kutoa muda kwa ajili ya mazungumzo.
Ijumaa, Trump alionyesha kuchoshwa na kasi ya mazungumzo hayo na kutishia kuweka ushuru wa asilimia 50.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alisema Von der Leyen alimwambia mkutano utafanyika haraka kuona iwapo wanaweza kufikia makubaliano, na baadaye akaandika kwenye Truth Social kuwa ilikuwa heshima yake kuongeza muda wa mwisho.
Von der Leyen awali alisema yuko tayari kuchukua hatua haraka ili kufikia makubaliano ya kibiashara na Marekani, lakini kwamba EU ilihitaji hadi tarehe 9 Julai kufanikisha makubaliano mazuri.
Katika maelezo kwa waandishi wa habari Ikulu ya White House Ijumaa mchana, saa chache kabla ya mazungumzo na Umoja wa Ulaya, Trump alisema alipanga kuongeza ushuru kwa bidhaa zote zinazoingia Marekani kutoka EU hadi asilimia 50 kufikia tarehe 1 mwezi Juni, akieleza kutoridhishwa na jinsi mazungumzo yalikuwa yakiendelea.
Baadaye siku hiyo hiyo ya Ijumaa, Mkuu wa Biashara wa EU Maroš Šefčovič alisisitiza kuwa Umoja huo umejitolea kufanikisha makubaliano ya haki.
Baada ya mazungumzo ya simu na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer na Waziri wa Biashara Howard Lutnick, walisema EU imejitolea kikamilifu kufanikisha makubaliano yatakayonufaisha pande zote mbili.