Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi wapiga kura wa nchi hiyo kwamba akishinda uchaguzi na kuwa Rais, Uchumi wa Tanzania utakua.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni jana Alhamisi Septemba 18, 2025 katika eneo Nungwi, Kaskazini Unguja, Zanzibar ambapo alisema ukuaji huo utwakuwa wa kiwango cha asilimia 7 mwaka wa kifedha wa 2026/27.
Rais Samia alisema hatua hiyo itaafikiwa kwa ushirikiano uliopo wa utekelezaji wa sera za uchumi na fedha kwa pande zote mbili za muungano ambazo ni Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar.
“Sera za kiuchumi na kifedha zimefanya kazi nzuri zaidi na tumeweza kukua, tulikuwa tunakua kwa asilimia 7 kabla ya Covid na kuporomoka kwa uchumi lakini Dkt. Mwinyi ameweza kurudi haraka kwenye asilimia saba,” alisema Samia.
Akiongeza kwamba Tanzania pia ina matumaini kwamba mwakani 2026/27 itarejelea kiwango hicho cha ukuaji cha asilimia 7 kama ilivyo Zanzibar.
Kulingana naye uchumi kwa Tanzania bara na Zanzibar uliyumba zaidi mwaka 2020 kutokana na janga la Uviko-19, kuporomoka kwa uchumi wa dunia pamoja na kupungua kwa misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo kabla ya jitihada kubwa kufanywa na Serikali mbili za Muungano na hivyo kuweza kuhimili misukosuko ya kiuchumi iliyokuwepo.
Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mnamo Oktoba 29, 2025 na hii ndiyo mara ya kwanza Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa anagombea wadhifa huo. Kipindi anachoendelea kuhudumu ni cha Hayati Rais John Pombe Magufuli.