Rais Samia aagiza sheria za Tanzania zitafsiriwe hadi Kiswahili

Kiongozi huyo wa Tanzania alitoa agizo hilo leo katika Ikulu ya Chamwino, kwenye hafla ya uzinduzi wa toleo la sheria za Tanzania zilizofanyiwa marekebisho la mwaka 2023.

Marion Bosire
2 Min Read
President Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza mwanasheria mkuu wa serikali akamilishe shughuli ya kutafsiri sheria za Tanzania kwa lugha ya Kiswahili.

Katika taarifa iliyotiwa saini na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais katika Ikulu Sharifa B. Nyanga, Rais Samia alisema tafsiri hiyo ihusishe pia toleo la sheria za Tanzania la Mwaka 2023.

Kiongozi huyo wa Tanzania alitoa agizo hilo leo katika Ikulu ya Chamwino, kwenye hafla ya uzinduzi wa toleo la sheria za Tanzania zilizofanyiwa marekebisho la mwaka 2023.

Aidha Rais Samia ameelekeza kwamba mipango ifanywe ya kuhakikisha upatikanaji wa rahisi wa nakala za toleo hilo hata kupitia kwa matumizi ya TEHAMA.

Lengo la kufanya hivyo kulingana naye, ni kuhakikisha kwamba wananchi wanazipata kwa urahisi kwenye mitandao ili wajifunze na kufahamu haki zao.

“Sheria ni kioo cha ustaarabu wa taifa, bila sheria zilizowekwa wazihaki haiwezi kupatikana, bila sheria kuwa wazi uhakika wa ulinzi wa haki ya raia unatoweka.” alisema Rais Samia.

Aliongeza kusema kwamba hali kama hiyo husababisha ukosefu wa amani na utekelezaji wa shughuli za kiuchumi kwa njia iliyojaa mashaka.

Kiongozi huyo wa Tanzania anaamini kukamilika kwa Toleo la Sheria zilizofanyiwa marekebisho kutarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa kuwa Sheria zote kuu 446 zimehuishwa, zinapatikana kwa pamoja na kwa urahisi na zimepangwa vizuri.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameagiza zoezi la marekebisho ya Sheria liwe likifanyika kila baada ya miaka 10 badala ya hali ya sasa ambapo limefanyika baada ya miaka 20 .

Share This Article