Rais Ruto: Ushirikiano kati ya Kenya na EU umepiga hatua kubwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto asema ushirikiano wa Kenya na EU umeimarika.

Rais William Ruto amesema ushirikiano kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya, EU unazidi kupiga hatua baada ya nyingine, hatua inayoimarisha uhusiano uliopo.

Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa ushirikiano huo umeshuhudiwa pakubwa katika sekta za biashara, uwekezaji, kukabiliana na Tabia Nchi, amani na usalama, elimu na kilimo, miongoni mwa nyingine.

Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi alipowaaga mabalozi ambao muda wao wa kuhudumu hapa nchini umekamilika, Rais Ruto alisema kuwa, ushirikiano kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya, uliimarika zaidi baada ya kutiwa saini kwa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi ulioanza kutekelezwa Julai 1,2024.

Kulingana na Rais, Makubaliano hayo, yalitoa fursa kwa wakenya kuuza bidhaa za Kenya kwenye soko la watu milioni 450 Ulaya, bila kutozwa ushuru.

Mabalozi hao ambao wanaondoka hapa nchini ni pamoja na Pirkka Tapiola wa Finland, Katarína Žuffa Leligdonová (Slovakia), Christina Diaz (Uhispania) na Caroline Vicine (Uswidi).

Rais aliwashukuru kwa jukumu walilotekeleza la kuzileta pamoja nchi hizo, huku akiwatakia ufanisi katika majukumu yao yanayofuata.

Share This Article