Rais William Ruto ametetea hatua yake ya kumuondoa aliyekuwa waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kwenye Baraza la Mawaziri, akisema kuwa Muturi alishindwa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na wanahabari katika Ikulu ndogo ya Sagana, kaunti ya Nyeri Jumatatu usiku, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa alipomteua Muturi kuwa Mwanasheria Mkuu, alitepetea kuwahudumia wakenya katika wadhifa huo, huku Muturi mwenyewe akimfahamisha Rais jukumu hilo lilikuwa ngumu kwake.
“Nilipatia JB Muturi kazi kama Mkuu wa Sheria, yeye mwenyewe alinielezea hii kazi kidogo inamlemea, kwa muda nikaona kweli kazi imemlemea, nikampatia kazi ya waziri,” alisema Rais Ruto.
Ruto alisema, baada ya kutafakari alimhamisha Muturi na kumpa kazi wa waziri, ambapo aliteuliwa kuwa waziri wa Utumishi wa Umma katika mabadiliko yaliyofanywa mwezi Agosti mwaka 2024.
Hata hivyo, kulingana na Rais Ruto, Muturi alisusia mikutano ya Baraza la Mawaziri, hatua iliyosababisha kutimuliwa kwake.
‘Nilimpatia Bwana Muturi kazi ya kuwa waziri. Hapo katikati akagoma kuja katika Baraza la Mawaziri. Ni mimi nilimfuta kazi au ni yeye alijifuta kazi?,” aliuliza Rais Ruto.
Rais Ruto alikuwa akijibu maswali kutoka kwa wanahabari, kabla ya kuanza ziara ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya kuanzia leo Jumanne.
Kiongozi wa taifa anatarajiwa kuzindua miradi ya maendeleo na kukagua ile ambayo tayari inaendelea, katika eneo hilo la Mlima Kenya.