Rais William Ruto amelisifu Shirika la Fedha Duniani (IMF), akisema kwa muda mrefu limefanikisha mageuzi makubwa ya kiuchumi hapa nchini.
Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa IMF imesaidia pakubwa kwa kutoa utaalam kwenye usimamizi wa madeni ya nje na usaidizi wa kiufundi katika sekta muhimu za uchumi wa taifa hili.
“Kupitia kwa usaidizi wa washirika wetu wa kimataifa, likiwemo Shirika la IMF, uchumi wa Kenya umepiga hatua kubwa na kusonga kutoka nafasi ya nane hadi sita barani Afrika,’ alisema Rais Ruto.

Rais Ruto aliyasema hayo aliposhiriki meza ya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva Jijini Washington nchini Marekani.
Kwenye mkutano huo, viongozi hao wawili walijadili kuimarisha ushirikiano, uwazi na usimamizi bora wa kiuchumi.
Rais Ruto yuko nchini Marekani kwa mualiko wa Rais Donald Trump, ambako atashuhudia kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.