Serikali ya taifa imeshirikiana na zile za kaunti pamoja na washirika wa maendeleo, kufanikisha mageuzi katika sekta ya afya kote nchini.
Rais William Ruto alisema lengo kuu la serikali ni kuhakikisha kila Mkenya anapata huduma za afya za ubora wa hali ya juu.
Aliyasema hayo leo Jumatato, alipopokea magari ya kuwabeba wagonjwa na vifaa vya matibabu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), katika Ikulu ya Nairobi.
Vifaa hivyo vitapelekwa katika hospitali saba za rufaa pamoja na kituo cha Kitaifa cha kukabiliana na dharura katika wizara ya fedha.
“Kaunti za Elgeyo Marakwet, Marsabit, Siaya, Samburu na Tana River, pia zitapokea magari ya kuwashughulikia wagonjwa ili kupiga jeki afya ya uzazi,” alisema Rais Ruto.
Aidha, kiongozi wa taifa alisema kuwa vifaa hivyo vya matibabu vitasaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na kuboresha utayari wa taifa hili kukabiliana na magonjwa kama vile Kipindupindu, Mpox na magonjwa mengine hatari kwa afya ya umma.