Serikali inatekeleza mikakati na mipango mbalimbali, kukabiliana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Hayo yamesemwa na Rais William.
Rais alidokeza kwamba, kwa muda mrefu taifa hili halijakuwa na mpango maalum wa kubuni nafasi za ajira.
Akizungumza Jumanne wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana katika kaunti ya Kakamega, Rais Ruto aliangazia mipango kama vile nyumba za bei nafuu, kazi za ughaibuni, vituo vya kidigitali vya kuwakuza vijana na ClimateWorx, kama miradi inayobuni nafasi za ajira kwa vijana hapa nchini.
“Changamoto kubwa zaidi miongoni mwa vijana,ni ukosefu wa ajira na fursa za kujiendeleza,” alisema Rais Ruto.
Katika hafla hiyo Rais alitoa hundi ya shilingi milioni 163, kupiga jeki makundi 816 ya vijana ambao wamepata nafasi za ajira ughaibuni.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, Waziri wa Michezo Salim Mvurya na Waziri wa Vyama vya Ushirika, Biashara ndogo na za Kadri Wycliffe Oparanya.