Rais Ruto, Rachel wawatakia watahiniwa mafanikio

Watahiniwa 996,000 watafanya mtihani wa kidato cha nne, KCSE mwaka huu. Watahiniwa 1,298,089 watafanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya sita, KPSEA wiki ijayo, huku 1,130,669 wakifanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya tisa (KJSEA).

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akiwa na Mama Rachel Ruto

Rais William Ruto na Mama wa Taifa Rachel Ruto wamewatakia watahiniwa wa mwaka huu mafanikio wanapoanza kufanya mitihani yao ya kitaifa. 

Kwenye ujumbe, Ruto na Mama Rachel wamewataka watahiniwa kuwa na imani kwamba wataibuka kidedea matokeo yatakapotangazwa kwani wamejiandaa vilivyo kuukabili mtihani huo.

“Mmejibidiisha, mmejiandaa vema, na sasa wakati umewadia. Anzeni mtihani huo kwa ujasiri, imani na kuwa na shabaha. Kenya inajivunia na kuwasherehekea katika kila hatua,” alisema Rais Ruto na Mkewe kwenye ujumbe huo.

Wanafunzi wa kidato cha nne walianza rasmi mtihani wa kitaifa (KCSE) wa mwaka 2025 jana Jumanne kwa kufanya mitihani ya mahojiano ya masomo ya Kifaransa, Kijerumani, Kiarabu, Lugha ya ishara ya Kenya na vitendo vya somo la muziki.

Mitihani ya masomo ya kuandikwa itaanza Novemba 4 na kukamilika Novemba 21, baada ya kukamilika kwa mitihani ya mahojiano na ya vitendo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani nchini (KNEC), David Njengere, amesema kuwa zaidi ya watahiniwa 996,000 watafanya mtihani huo.

Njengere alitoa hakikisho kuwa maandalizi ya kina yamefanyika ili kuhakikisha mtihani huo unaendelea kwa utulivu na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaopatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani.

Wakati huo huo, wanafunzi 1,298,089 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya sita, KPSEA wiki ijayo, huku 1,130,669 wakitarajiwa kufanya mtihani wa kitaifa wa Gredi ya tisa (KJSEA).

Share This Article