Rais William Ruto amemwomboleza Jaji wa Mahakama ya Upeo Mohammed Ibrahim aliyeaga dunia jana Jumatano, akimtaja kuwa mpenda amani, mtetezi wa haki za binadamu na aliyepigia debe demokrasia.
Kupitia ukurasa wake wa X, kiongozi wa taifa alisema Jaji Ibrahim aliweka historia kwa kuwa wa kwanza kutoka jamii yake kujiunga na Mahakama Kuu ya Kenya.
“Kwa niaba yangu na Wakenya wote kwa jumla, natuma rambirambi kwa familia, marafiki, wafanyakazi wenza na idara yote ya sheria,” alisema Rais Ruto.
Kwa upande wake, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alisema kifo cha Jaji Ibrahim kimeacha pengo kubwa kwenye Mahakama ya Upeo ambalo itakuwa vigumu kulijaza ikizingatiwa jinsi alivyojitolea kuhakikisha haki inapatikana.
“Tunapoomboleza , natuma rambirambi kwa familia ya Ibrahim ambaye alikuwa mtetezi wa haki za binadamu. Mungu ailaze roho yake mahali pema,” aliomboleza Mudavadi.
Jaji Ibrahim alifariki Jumatano baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Amemwacha mjane na watoto wanne.