Rais William Ruto kwa sasa anahutubia taifa kutoka majengo ya bunge katika kikao cha pamoja kitakachowaleta pamoja wabunge wa Bunge la Taifa na Maseneta.
Rais Ruto aliwasili katika majengo ya bunge majira ya 8:30 alasiri na kuanza kuhutubia taifa majira ya saa tisa alasiri baada ya kukagua gwaride la heshima.
Hii ni mara ya tatu kwa Rais Ruto kuhutubia taifa tangu alipoingia madarakani.
Akihutubia kikao hicho, Rais Ruto alikiri kuwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita hakijakuwa rahisi, lakini sasa mambo yanaanza kutengemaa.
Rais Ruto akitaja kupungua kwa mfumko wa bei uliokuwa asilimia 9 hadi 4.6, kuimarika kwa sarafu ya Kenya, na kuongezeka kwa Pato Ghafi la Taifa hadi dola bilioni 133 na kuifanya Kenya kuwa nchi ya sita iliyostawi zaidi barani Afrika kuwa baadhi ya mafanikio ya utawala wake.
Kulingana na Rais, mafanikio hayo yametokana na mipango madhubuti iliyowekwa na utawala wake.
Miongoni mwa mipango mingine ambayo Rais amegusia ni Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, ujenzi wa nyumba za bei nafuu, na utekelezaji wa miundombinu mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara na viwanja vya michezo kama vile Talanta.
Aidha, kiongozi wa nchi anatarajiwa kugusia masuala ya usalama hususan katika maeneo ambayo yamekumbwa na ukosefu wa usalama kama vile North Rift na ufadhili wa sekta ya elimu ambayo imekumbwa na changamoto si haba ukiwemo mgomo wa hivi karibuni wa wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma.
Naibu Rais Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri na Mabalozi wa nchi mbalimbali ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria kikao hicho.