Rais Ruto kuhudhuria mkutano wa TICAD 9 nchini Japani

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ataondoka nchini leo Jumatatu jioni kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo juu ya Maendeleo ya Afrika (TICAD).

Mkutano huo unaoandaliwa mjini Yokohama ni wa 9 tangu kuasisiwa kwake.

Wakati za ziara yake nchini Japani, Ruto atashiriki mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Shigeru Ishiba kuhusiana na masuala mbalimbali.

“Mazungumzo hayo yataangazia miradi muhimu ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa bandari ya Mombasa, uendelezaji wa barabara ya eneo la bandari la Mombasa, Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Dongo Kundu, na mifumo ya kisasa ya usafiri jijini Nairobi,” ilisema taarifa kutoka kwa Msemaji wa Ikulu ya Nairobi, Hussein Mohamed.

“Nyanja zingine za ushirikiano zinajumuisha kilimo, misitu, na mabadiliko ya tabia nchi, huku Japani ikiwa tayari inasaidia katika utengenezaji wa miundombinu ya unyunyiziaji wa mashamba maji na juhudi za upanzi upya wa miti.”

Kwenye mkutano wa TICAD 9, Rais Ruto anatarajiwa kutoa wito wa utangamano na uunganishaji wa kina zaidi barani Afrika ili kuhakikisha bara hilo linafikia upeo wa uwezo wake kiuchumi.

Atasisitiza umuhimu wa Makubaliano ya Biashara Huru barani Afrika (AfCFTA) kama kichocheo kikuu cha ukuaji jumuishi, na wakati huohuo kutoa wito wa uondoaji wa vizuizi vya kibiashara.

Share This Article