Rais Ruto kuelekea China Jumanne

Ubalozi wa China nchini Kenya ulitangaza Alhamisi kwamba Rais Ruto alialikwa rasmi na Rais wa China Xi Jinping.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto anatarajiwa kuelekea China Jumanne kwa ajili ya ziara rasmi, anapotafuta kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Kenya na China.

Akizungumza wakati wa mahojiano na shirika la habari ka China, China Media Group, Rais Ruto alisema anatizamia kujenga uhusiano mwema kati ya watu wa China na watu wa Kenya.

Kulingana naye, uhusiano huo umekuwepo kwa muda mrefu na lengo lake kuu ni kuuhuisha na kuongeza kasi katika ukuzaji wa uhusiano wa pande zote mbili.

Ziara hiyo ya siku tano, itaangazia pia kukamilishwa kwa miradi inayoendelea chini ya ushirikiano wa Kenya na China pamoja na namna ya kuanzisha miradi mingine ambayo itachochea na kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili.

Ubalozi wa China nchini Kenya ulitangaza Alhamisi kwamba Rais Ruto alialikwa rasmi na Rais wa China Xi Jinping.

Mojawapo ya miradi itakayojadiliwa wakati wa ziara ya Rais nchini China ni upanuzi wa barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Nakuru kwa gharama ya shilingi bilioni 190.

Rais Ruto anarejea Chinamiezi kadhaa baada ya kuwa nchini humo kwa ajili ya kongamano la ushirikiano kati ya China na Afrika – FOCAC lililoandaliwa Septemba 2024.

Wakati huo wa FOCAC, Kenya pia ilitafuta kuafikia makubaliano kadhaa muhimu pamoja na uwekezaji ambao utafaidi nchi zote mbili kwa miaka mingi ijayo.

Share This Article