Rais William Ruto leo Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi, alizindua usambazaji wa Vifaa vya Afya katika juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Akiongea wakati wa hafla hiyo, kiongozi wa taifa alisema vifaa hivyo ni dhihirisho la kujitolea kwa serikali kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha wakenya wamenufaika na huduma bora za afya.
“Tunaweka Vifaa vya Afya vya Kisasa katika vituo vya afya, kuhakikisha vinapata vifaa vya kutambua na upatikanaji wa teknoloji za matibabu kwa wote,” alisema Rais Ruto.
Aidha, alisema mradi huo ni jitihada ya pamoja inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Afya na Baraza la Magavana, kwa lengo la kuhakikisha vituo vya afya vya umma katika viwango vyote vina teknolojia za kisasa za matibabu.
Mradi huo pia utatoa vifaa kama vile mitambo ya kufanikisha uchunguzi wa kina mwilini, upasuaji pamoja na maabara huku pia ukiwezesha utoaji mafunzo na msaada wa ukarabati.
Mradi huo unapaniwa kuhakikisha miundombinu ya kisasa katika utoaji huduma za matibabu huku ikifanikisha ugunduzi wa mapema wa magonjwa na matibabu ya maradhi katika vituo vya afya vya umma.