Rais William Ruto amesema ipo haja ya ushirikiano wa pamoja, ili kutimiza ajenda ya mageuzi ya taifa hili.
Kiongozi huyo wa taifa alitoa wito wa kuweka kando siasa ambazo zinaleta migawanyiko, huku akipendekeza ushirikiano wa kitaifa, ili kuhakikisha ustawi wa taifa hili kwa manufaa ya raia wake.
Akizungumza Ijumaa alipokuwa mgeni wa mwenyekiti wa chama cha KANU Gideon Moi wakati wa mkutano wa mashinani wa chama hicho katika kaunti ya Nakuru, Rais Ruto alidokeza kuwa ajenda yake ni kuwaunganishja Wakenya wa matabaka mbalimbali na kulifanya taifa hili kuwa miongoni mwa chumi zilizoendelea zaidi ulimwenguni.
“Tunapaswa kupiga kumbo siasa za migawanyiko na kuwa washirika wa umoja wa kitaifa,” alisema Rais Ruto.
Alipongeza chama cha KANU kwa kukubali kufanya kazi kwa pamoja na serikali ya Kenya Kwanza chini ya mfumo wa serikali jumuishi.
“Ninafuraha kwamba chama cha KANU chini ya uongozi wa Gideon Moi utashirikiana nasi, kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hili,” aliongeza Rais Ruto.
Mkutano huo wa viongozi hao unajiri siku moja baada ya Gideon Moi kujiondoa kuwania wadhifa wa Seneta wa Baringo kwenye uchaguzi mdogo wa mwezi Novemba.
Rais alisifia hatua ya Moi ya kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho, huku akimpigia debe muwaniaji wa chama cha UDA Vincent Kiprono Chemitei.