Rais Ruto azungumza baada ya ushinde wa AUC

Uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Afrika uliandaliwa jana Jumamosi Februari 15, 2025, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameshukuru uongozi wa Umoja wa Afrika AU, baada ya ushinde wa mwaniaji wa Kenya Raila Odinga, wa uenyekiti wa tume ya Umoja huo AUC.

Uchaguzi wa viongozi wa Umoja wa Afrika uliandaliwa jana Jumamosi Februari 15, 2025, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Katika taarifa fupi kupitia mitandao ya kijamii baada ya uchaguzi hio, Ruto alishukuru AU kwa kutoa fursa kwa Raila Odinga kuonyesha maono na vipaumbele vyake kwa Bara Afrika.

“Huku matokeo ya uchaguzi huu yakikosa kupendelea mwaniaji wa Kenya, ninataka kushukuru uongozi wa hili bara letu.” aliandika Rais Ruto.

Rais Ruto alitumia fursa hiyo pia kumpongeza mwenyekiti mpya wa tume ya Umoja wa Afrika AUC Mahmoud Youssouf na naibu wake Selma Haddadi.

“Mna imani ya mkusanyiko wa Umoja wa Afrika na Kenya inaahidi kuwaunga mkono mnapoendesha tume ya Umoja wa Afrika hadi viwango vingine.” Alisema Rais.

Kiongozi huyo wa Kenya alisisitiza kwamba uchaguzi huo haukuwa unalenga watu binafsi au mataifa fulani bali ulikuwa unahusu mustakabali wa pamoja wa bara Afrika.

“Mustakabali huo unasalia kuwa unaong’aa na pamoja tutaendelea kushirikiana kwa ajili ya Afrika yenye Umoja, mafanikio na ushawishi katika jukwaa la ulimwengu.” alimalizia kusema Rais Ruto.

Wawaniaji wa wadhifa huo walikuwa watatu, Raila Odinga wa Kenya, Mahmoud Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar.

Share This Article