Rais William Ruto amewazomea wanaokosa michango anayotoa kwa makanisa akisema ataendelea kusaidia makanisa kama njia ya kutokomeza ukosefu wa maadili unaoshuhudiwa nchini.
Akizungumza katika ibada jana huko Eldoret, Rais alisema vijana nchini wanakabiliwa na changamoto kama matumizi ya dawa za kulevya, unywaji pombe kupita kiasi na usherati.
Kutokana na hilo, kiongozi wa nchi anahisi kuna haja ya kuimarisha makanisa ili yaweze kutoa maelekezo bora ya kimaadili kwa vijana.
Usemi wa Rais unajiri wakati ambapo amekosolewa na wengi kwa kutoa michango ya kiasi kikubwa cha pesa kwa makanisa ukiwemo mchango wa shilingi milioni 20 kwa kanisa la Jesus Winner Ministry huko Roysambu wiki iliyopita.
Mapema jana, maafisa wengi wa polisi walikuwa nje ya kanisa hilo baada ya baadhi ya vijana kutishia kufanya maandamano huko kufuatia mchango huo wa milioni 20.
Wakati huo huo, Rais Ruto amesema kwamba Kenya imepiga hatua katika maendeleo katika nusu ya kwanza ya muhula wa serikali ya Kenya Kwanza.
Alitaja utekelezaji uliofanikiwa wa mipango mbali mbali, ukuaji wa sekta ya kilimo na uchumi ulioimarika huku akiahidi mabadiliko zaidi katika miaka ijayo.