Rais Ruto azindua upanuzi wa barabara ya Nairobi–Mau Summit

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amezindua rasmi upanuzi wa barabara za kutoka Nairobi kuelekea Mau Summit na Nairobi kuelekea Maai Mahiu hadi Naivasha kuwa za safu mbili mbili.

Akizungumza huko Kamandura kaunti ya Kiambu wakati wa uzinduzi huo, kiongozi wa nchi alisema lengo kuu la mradi huo ni kupunguza msongamano na kuboresha usalama katika ukanda wa Magharibi.

Katika hotuba yake, Rais alisema kwamba watumizi wa sehemu hizo za barabara za umbali wa kilomita 175 na kilomita 58 wamekuwa wakikumbwa na ucheleweshwaji mkubwa wa magari na ajali, ambazo zimenyakua mamia ya maisha katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2024 pekee, Rais alibainisha kuwa watu 284 walifariki katika barabara hizi, ikilinganishwa na 168 mwaka 2023.

Mradi huo wa shilingi bilioni 200 unatarajiwa kupunguza msongamano, kupunguza ajali za barabarani, na kuboresha muunganiko kuelekea eneo la Magharibi, hivyo kuchochea biashara na shughuli za kiuchumi ndani ya Kenya na nje ya mipaka yake.

Rais Ruto alieleza kuwa hatua hii ni hatua kubwa kuelekea mfumo salama, bora na wenye ufanisi zaidi wa usafiri kwa nchi.

Kiongozi wa nchi alibainisha kwamba pesa zitakazotumika kwenye mradi huo utakaopunguza muda wa safari za kuelekea magharibi mwa nchi, ni dola bilioni 1.54, sawa na shilingi bilioni 200.

Share This Article