Rais William Ruto leo Ijumaa amezindua rasmi Mradi wa Kitaifa wa Kuwapa Vijana Fursa za Kujiendeleza (NYOTA).
Uzinduzi wa mradi huo ulifanyika katika uwanja wa michezo wa Mumias Sports Complex, kaunti ya Kakamega.
“Mradi huo na vipengele vingine pia unatoa uanagenzi na furza za ajira, unatambua mafunzo ya awali katika ujuzi mbalimbali, unahamasisha vijana kuweka akiba, na kujenga uwezo wa vijana kufanya biashara na serikali,” alisema Rais Ruto wakati wa uzinduzi huo.
“Uzinduzi wa kipengele cha msaada wa biashara wa shilingi bilioni 5 wa (NYOTA) ni mwanzo wa hatua kubwa katika uwezeshaji vijana nchini, hatua madhubuti ya kupanua fursa kwa vijana katika biashara.”

Rais Ruto akielezea imani kuwa mradi huo utasaidia vijana wajasirimali 110,000 kukuza biashara zao, kuboresha maisha yao, na kubuni fursa kwa ajili ya wengine.
“Kwa kusambaza msaada wa shilingi 50,000 kwa wafanyabiashara vijana 70 katika kila wadi 1,450, mpango huo unahakikisha ujumuishaji na usawa kote nchini,” alisema Ruto.
Aliongeza kuwa kupitia teknolojia ya kidijitali, mpango huo utahakikisha uwazi, usawa na upatikanaji wa fedha kwa urahisi kwa wote watakaonufaika.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Gavana wa Vihiga Dkt. Wilber Ottichilo.