Rais William Ruto leo Jumatatu amezindua awamu ya pili ya usafishaji mto Nairobi itakayoshirikisha kuwaajiri vijana zaidi ya 18,000.
Vijana hao watajenga kilomita 54 za mabomba ya kupitisha maji taka kando ya mto huo.
Ruto ameongeza kuwa serikali itanunua malori 50 mapya kwa shughuli hiyo, akifafanua kuwa mshahara wa vijana watakaotekeleza mradi huo utaongezwa na utakuwa ukilipwa kwa wakati.
Rais aliyesema hayo katika uwanja wa Kamukunji katika kaunti ya Nairobi, wakati wa kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja miongoni mwa viongozi wengine wa kaunti hiyo.
Kiongozi wa nchi alikariri kuwa tayari vijana 20,000 wanashirikishwa katika awamu ya kwanza ya kusafisha mto Nairobi.
Vijana hao wanaofanya kazi kwa wiki mbili, wakipishana na kundi lingine, watalipwa shilingi 500 kwa siku huku wasimamizi wao wakilipwa shilingi 550 kwa siku.