Rais William Ruto siku ya Jumatatu alipokea vyeti vya utambulisho vya Mabalozi na Makamishna sita wakuu wapya katika Ikulu ya Nairobi, katika hafla inayonuiwa kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Mabalozi hao ni Adarsh Swaika (India), Vincenzo Del Monaco (Italy), Verónica García Gutiérrez (Costa Rica), Paul Evans Aidoo (Ghana), Gia Matcharadze (Georgia), na Lilly Stella Ngyema Ndong (Gabon).
Rais alisema Kenya inajizatiti kuimarisha uhusiano wa kimataifa kote duniani, akisisitiza kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha biashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha maendeleo endelevu.
Alisema kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kutafanikisha ukuaji wa kiuchumi wa taifa hili na kufanya Kenya kuwa mshirika muhimu kwenye maswala ya kimataifa.
Rais Ruto alisema ushirikiano huo ni jitihada za kuhakikisha kuna manufaa kwa taifa hili kutokana na kuimarishwa kwa uchumi kupitia ushirikiano kwenye maswala kama vile teknolojia, miundo-mbinu na uongozi.