Rais Ruto awaongoza Wakenya kumuomboleza Dkt. Phoebe Asiyo

Tom Mathinji
2 Min Read
Mbunge wa zamani Dkt. Phoebe Muga Asiyo, afariki dunia.

Rais William Ruto amemuomboleza aliyekuwa mbunge wa Karachuonyo Dkt. Phoebe Muga Asiyo, akimtaja kiongozi mjasiri aliyepigania usawa wa kijinsia.

“Sauti yake ilitekeleza wajibu muhimu wa kupigia debe ujumuishaji wa wanawake katika ulingo wa kisiasa,” alisema Rais Ruto kupitia ukurasa wake wa X Alhamisi jioni.

Kwa upande wake waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alimkumbuka Dkt. Asiyo kuwa kiongozi shupavu aliyetetea elimu ya mtoto wa kike, usawa wa kijinsia na haki za wanawake nyakati ambapo ilikuwa vigumu kwa wanawake wengi kuchukua jukumu kama hilo.

“Urithi wake umekitwa kwenye maendeleo ya taifa hili kuhakikisha usawa na heshima kwa wote,” alisema Mudavadi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ametuma risala za rambirambi kwa jamii ya familia ya Dkt. Phoebe Asiyo, akimtaja mwalimu aliyebadilisha maisha ya wavulana na wasichana na kufanikisha marekebisho makubwa kwa taifa hilo.

Huku akituma rambirambi hizo kwa niaba ya familia ya Jaramogi Oginga Odinga, Raila alimtaja mbunge huyo wa zamani kuwa aliyeonyesha umahiri wake baada ya kupanda ngazi kutoka kwa kuwa mwalimu hadi Afisa Mkuu katika idara ya Magereza Nchini.

“Phoebe aliwatengenezea njia wanawake wengi kutokana na mano bora wa maisha yake. Tunaitakia familia yake amani wakti huu mgumu.

Alifariki dunia akiwa North Carolina nchini Marekani. Tangazo la kifo chake lilitolewa na familia yake.

Share This Article