Rais William Ruto amesisitiza haja ya hatua za pamoja na za haraka za kukabiliana na njaa na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote.
Akihutubia kongamano kuhusu kuhakikisha ulimwengu usiokuwa na njaa jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, Rais aliangazia takwimu zinazoonyesha kwamba tatizo la njaa linazidi kuongezeka.
Kulingana naye, tatizo hilo linaongezwa na ukosefu wa usawa wa kiuchumi, migogoro na mabadiliko ya tabianchi.
Katika hotuba hiyo, Ruto ualisema kwamba watu wapatao milioni 733 walikabiliwa na njaa mwaka jana, ambapo bara Afrika liliathirika sana huku mtu mmoja kati ya watano akikumbwa na ukosefu wa chakula.
Aliongeza kwamba watu zaidi ya milioni 2.8 ulimwenguni hawawezi kumudu lishe bora, akisisitiza athari pana za njaa zinazojumuisha afya mbaya, tija iliyopungua na kupotea kwa uwezo.
“Kongamano hilo ni muhimu kwa sababu linatukutanisha ili tuweze kuangazia hali ya jukumu letu la pamoja la kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama, cha kutosha na chenye ubora kwa wote,” alisema Rais Ruto.
Tatizo la njaa alilotaja kuwa umaskini uliokithiri wa ustawi, alisema lisiposhughulikiwa haraka, jamii ya kimataifa itakosa kuafikia lengo la pili na maendeleo endelevu ambalo ni kutokuwepo kwa njaa.
Theluthi moja ya chakula cha binadamu kinachozalishwa alisema huwa kinaharibika au kupotea kila mwaka hali ambayo kulingana naye haikubaliki kwani ni hasara ya dola trilioni 1 kila mwaka.
Kiongozi huyo wa Kenya aliangazia uwekezaji wa Kenya katika mabadiliko ya kilimo na maendeleo ya kiteknolojia yanayolenga kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Uwekezaji katika mipango ya lishe shuleni alisema utaongezwa mara dufu kwa lengo la kuhakikisha kwamba watoto wanapata lishe bora na mifumo ya mashinani ya chakula inapigwa jeki.
Ruto alitambua kwamba mipango ya kushughulikia njaa ulimwenguni inahitaji kujitolea na ushirikiano kati ya mashirika ya kimataifa, serikali mbali mbali na wadau.
Kongamano hilo kwa jina “World Without Hunger” limekutanisha viongozi na wadau kutoka kote ulimwenguni ili kuangazia utatuzi wa mojawapo ya changamoto kuu za binadamu na kuhakikisha uendelevu.