Rais Ruto atoa ahadi mpya kwa Wakenya kwenye maadhimisho ya Leba Dei

Alitoa ahadi hizo katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wafanyakazi katika uwanja wa Uhuru Gardens Nairobi.

Marion Bosire
3 Min Read

Rais William Ruto leo ameongoza maadhimisho ya awamu ya 60 ya sikukuu ya wafanyanyakazi ulimwenguni almaarufu “Labour Day” ambapo alidondoshea wafanyakazi ahadi kadhaa.

Ahadi za kiongozi wa nchi zinaambatana na mabadiliko ya sera yanayolenga kuboresha haki za wafanyakazi, mapato yao na fursa za ajira kwa wakenya wengine wengi.

Katika hotuba yake kwenye uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi, Rais Ruto alitangaza kwamba uchakataji wa nafuu ya kodi utafanywa kabla ya kuwasilishwa kwa kodi na hivyo kuinua kiwango cha mshahara.

Waajiri sasa wanahitajika kutumia nafuu za kodi na misamaha ya kodi wanapochakata kodi ya Pay As You Earn (PAYE), na hivyo kukomesha mtindo wa sasa ambapo wafanyakazi hudai nafuu za kodi na misamaha ya kodi kutoka kwa shirika la ukusanyaji ushuru nchini KRA.

“Badiliko hili litafaidi wafanyakazi mara moja na hivyo kuongeza ufanisi wao” alisema Rais kwenye hotuba yake.

Kwa waliostaafu, Rais alitangaza kwamba malipo yao ya kustaafu hayatatozwa kodi tena hatua anayosema inalenga kutambua huduma na hadhi ya wastaafu kote nchini.

Rais Ruto aliahidi wamiliki wa biashara ndogo kwamba mifumo ya kodi itarahisishwa na hivyo kuwawezesha kuondoa gharama ya vifaa vya kila siku katika mwaka wa kuvinunua.

Badiliko hilo linalenga kupunguza kucheleweshwa kwa uafikiaji wa nafuu ya kodi na kurahisisha uzingatiaji kwa wamiliki wa biashara ndogo.

Katika elimu Rais Ruto alifichua kwamba shikingi bilioni 2.4 zimetengwa kwa ajili ya kuajiri walimu wanagenzi elfu 20 kuanzia Januari 2026.

Kiongozi wa nchi aliangazia pia upanuzi wa uwezo wa wakenya kuafikia soko la kimataifa la ajira ambapo alitangaza kufunguliwa kwa afisi ya afisa wa Leba jijini Berlin, nchini Ujerumani.

Afisi hiyo itakuwa kitovu cha makubaliano ya pande mbili ya leba katika eneo zima la Umoja wa Ulaya. Kulingana na Rais wakenya laki mbili walipata fursa za ajira ughaibuni mwaka jana na serikali inapania kutafuta fursa zaidi.

Rais Ruto aliagiza wizara ya leba ihakikishe kwamba wanaofanya kazi chini ya mikataba ya nje wanakubaliwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili wanufaike na mifumo ya majadiliano ya pamoja ya kazi.

Ruto aliahidi kwamba Kenya itaridhia maazimio ya mikutano miwili ya shirika la kimataifa la Leba ILO ili kuimarisha ulinzi kwa wafanyakazi walio katika hatari.

Azimio la kwanza ILO Convention 189 linalinda haki za wafanyakazi wa nyumbani na azimio la ILO Convention 190 linalenga kutokomeza vurugu na unyanyasaji katika maeneo ya kazi.

Share This Article