Rais Ruto atetea ushirikiano wake na Raila Odinga

Rais alisema makubaliano hayo ni kwa manufaa kwa kitaifa na yanalenga kuhakikisha uthabiti wa kisiasa nchini.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto kwa mara nyingine ametetea ushirikiano kati yake na kinara wa ODM Raila Odinga akipuuzilia mbali shutuma za usaliti kutoka kwa washirika wa pande zote mbili.

Akizungumza jana katika ibada ya Pasaka ya madhehebu mbalimbali huko Ntulele, Kaunti ya Narok, Rais alisema makubaliano hayo ni kwa manufaa kwa kitaifa na yanalenga kuhakikisha uthabiti wa kisiasa, kuimarika kwa uchumi na mabadiliko ya kitaasisi.

Matamshi ya Ruto yanafuatia hali ya kutoridhika inayoongezeka miongoni mwa baadhi ya wanachama wa muungano wake tawala wa Kenya Kwanza na upande wa ODM, ambao wanachukulia mkataba huo kama usaliti wa mamlaka yao ya uchaguzi.

Katika ibada hiyo ya jana, viongozi wa jamii ya maasai waliahidi kuhimiza jamii hiyo kumuunga mkono rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wakisema wameafikiana kuhusu swala hilo.

Katika tangazo la pamoja viongozi hao walikariri imani ya jamii hiyo katika uongozi na ajenda ya maendeleo ya rais.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alijitolea kutafuta takriban kura milioni- 1.4 za jamii ya Maasai kuwaunga mkono rais Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga.

Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu na mwenzake wa Kajiado Joseph Ole Lenku nao walisema rais amedhihirisha azma yake ya kuinua jamii zilizotengwa na kushughulikia tofauti za muda mrefu za kimaendeleo katika kaunti za wanaozungumza lugha ya Maa.

Share This Article