Rais wa Kenya William Ruto, alitoa hotuba nzito katika mazungumzo ya suluhu za ngazi ya juu kuhusu Ufadhili wa masuala ya tabianchi jijini New York, akitoa wito kwa dunia kubadili mwelekeo kuelekea mifumo ya ufadhili wa hali ya hewa inayozingatia haki na utekelezaji.
Akizungumza wiki chache tu baada ya Mkutano wa Hali ya Hewa wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ruto alieleza jinsi mataifa ya Afrika yanavyobeba mzigo mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi licha ya kuwa na mchango mdogo katika kusababisha tatizo hilo.
Rasilimali za ndani ni “kutokuwa na haki wazi” na kuna hatari ya kuyadhoofisha zaidi mataifa dhaifu kiuchumi.
“Afrika inapoteza takriban dola bilioni 90 kila mwaka kupitia mianya ya kifedha haramu — fedha ambazo zingetumika kukabiliana na changamoto za hali ya hewa,” alisema Ruto, akihimiza kuungwa mkono kwa Mkataba wa Kodi wa Umoja wa Mataifa ili kuanzisha mfumo wa kodi wa kimataifa ulio wa haki.
Rais Ruto alielezea uwezo wa Afrika kuwa kitovu cha viwanda vya kijani, vyenye nishati mbadala na rasilimali asilia. Alitaja mikakati mipya kama Mpango wa Kiviwanda wa Afrika wa Kijani (AGII) na Ushirikiano wa Kuendeleza Nishati Jadidifu Afrika (APRA) kama ishara ya kujitolea kwa bara hilo kwa maendeleo endelevu.
Pia alifichua kuwa taasisi nane kuu za kifedha barani Afrika zimesaini makubaliano ya ushirikiano ya kufungua uwekezaji wa dola bilioni 100 katika sekta ya kijani, lakini akasisitiza haja ya ushirikiano wa kimataifa, mikakati ya kupunguza hatari, na matumizi ya fedha za umma kuharakisha juhudi hizo.
“Muda hauko upande wetu,” Ruto alionya. “Lazima tuchukue hatua kwa ujasiri na kwa pamoja, ili kugeuza changamoto ya tabianchi kuwa fursa kubwa ya kizazi chetu.”