Rais Ruto asema serikali imejitolea kuimarisha mfumo wa afya

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba serikali imejitolea kuimarisha mpango wa huduma bora za afya kwa wote UHC ili kuhakikisha huduma bora na faafu kwa wakenya.

Akizungumza jana huko Kikuyu katika mazishi ya Mzee Isaac Ichung’wah Ngugi, babake kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah, kiongozi wa nchi alisema kwamba serikali inajitahidi kuboresha mfumo wa afya.

Kulingana naye, lengo kuu la jitihada hizo ni za kuhakikisha mpango huo wa huduma bora za afya kwa wote unaafikiwa kikamilifu.

Rais Ruto aliwataka wakenya kuunga mkono mipango mbali mbali ya serikali ambayo inalenga kuboresha maisha yao.

Alimtaja marehemu Mzee Ngugi kuwa mtu mzuri ambaye aliishi maisha mema alipokuwa ulimwenguni, akiahidi kwamba serikali itasimama na familia yake wakati huu wa majonzo.

Ruto alisema wengi watamkosa mzee huyo kutokana na maisha yake ya kipekee.

Mzee Isaac Ichung’wah Ngugi aliaga dunia Septemba 5, 2025, akiwa na umri wa miaka 105.

Share This Article