Rais Ruto asaini miswada ya ulinzi wa jamii na mkinzano wa maslahi

Rais Ruto alitia saini miswada hiyo miwili katika Ikulu ya Nairobi mapema leo Jumatano.

Dismas Otuke
1 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto ametia saini kuwa sheria Mswada wa Ulinzi wa Jamii, 2025 na Mswada wa Mkinzano wa Maslahi, 2025. 

Rais Ruto alitia saini miswada hiyo miwili katika Ikulu ya Nairobi mapema leo Jumatano.

Akiutia saini kuwa sheria Mswada wa Mkinzano wa Maslahi, Ruto aliitaja sheria hiyo mpya kuwa hatua yenye ujasiri katika kupambana na zimwi la ufisadi nchini.

“Inaweka sheria bayana kwamba maafisa wa umma wanapaswa kutoa huduma kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji,” alisema kiongozi wa taifa.

Kwa upande mwingine, Ruto alisema Mswada wa Ulinzi wa Jamii unaunda mpangokazi mmoja uliojikita kwenye haki na kuhakikisha msaada usiokuwa wa mchango kwa Wakenya wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali maishani.

Mswada huo unalenga kuleta usawa katika makundi mbalimbali ya kijamii na uwazi katika utumishi wa umma.

Uliwasilishwa na kiongozi wa walio wengi bungeni Kimani Ichung’wah na kuidhinishwa Aprili 30 mwaka huu.

Baadaye, ulipitishwa na bunge la Seneti bila kufanyiwa mabadiliko tarehe 23 mwezi huu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Maspika Moses Wetang’ula na Amos Kingi, viongozi wa wengi pamoja na viranja wa mabunge yote mawili na Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, Dkt. David Oginde.

 

Share This Article